Ni zamu ya Profesa Kameri Mbote kuhojiwa kwa wadhifa wa jaji mkuu

0

Mahojiano ya kumtafuta jaji mkuu mpya yanaingia siku yake ya pili huku Profesa wa maswala ya kisheria Kameri Mbote akifika mbele ya tume ya huduma za mahakama (JSC) kuelezea ni kwa nini anatosha kumrithi mstaafu David Maraga.

Profesa Mbote ni mzaliwa wa kaunti ya Murang’a mwaka 1963 na ana uzoefu wa zaidi ya miaka thelathini katika maswala ya kisheria.

Kwa sasa yeye ni muhadhiri wa masomo ya kisheria katika chuo kikuu cha Nairobi kazi ambayo amekuwa akiifanya tangu mwaka 2011.

Jaji wa mahakama kuu Said Juma Chitembwe alifungua ukurasa wa mahojiano hayo akisema ana uwezo wa kumrithi Maraga kwa sababu ya uzoefu wake katika idara ya mahakama.

Amesema alichangia pakubwa katika kupunguza mrundiko wa kesi mahakamani alipohudumu katika mahakama za Kakamega, Malindi, Marsabit na Migori.

Jaji Chitembwe aidha aliahidi kuhakikisha kuwa kesi za ufisadi zinasikilizwa kwa haraka kinyume na ilivyo kwa sasa ambapo zinachukua muda mrefu.

Watu 10 wameorodheshwa kuhojiwa kwa wadhifa huo akiwemo majaji; Nduma Nderi, William Ouko, Martha Koome, Marete Njagi na mawakili Philip Murgor, Fredrick Ngatia, Patricia Mbote, Moni Wekesa na Alice Yano.

Awali

Jaji wa mahakama kuu Antony Mrima alidinda kutoa agizo linalositisha  mahojiano yanayoendelea kumtafuta mrithi wa David Maraga kama jaji mkuu.

Katika uamuzi wake, Jaji Mrima ameelekeza kesi hiyo kwa kaimu jaji mkuu Philomena Mwilu kubuni jopo la majaji watatu kusikiliza na kutoa uamuzi.

Mrima anadokeza kwamba kesi hiyo, inaibua maswala yenye uzito wa kikatiba na iNApaswa kusikilizwa na jopo la majaji.

Mlalamishi Tolphin Nafula ameishtaki tume ya huduma za mahakama (JSC) akipinga kuwepo kwa Olive Mugenda kama mwenyekiti tume hiyo akihoji kuwa naibu jaji mkuu Philomena Mwilu ndiye anapaswa kushikilia wadhifa huo.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here