NACADA yamkabili mlanguzi na kunasa bangi Molo

0

Mamlaka ya Kitaifa ya kukabili matumizi ya Pombe na Dawa za Kulevya (NACADA) imenasa bangi inayokadiriwa kuwa ya dhamani ya shilingi milioni moja mjini Molo kaunti ya Nakuru kufuatia operesheni ya kijasusi.

Operesheni hiyo ya pamoja ya vitengo mbalimbali ilifanyika usiku wa Jumatatu tarehe 2 Machi 2026 ikihusisha maafisa wa NACADA na maafisa wa polisi kutoka Molo.

Operesheni hiyo ilifanikiwa baada ya maafisa kupokea taarifa kutoka kwa umma kuhusu mshukiwa wa ulanguzi aliyeaminika kuwa alikuwa akisafirisha bangi hiyo kutumia gari moja aina ya probox.

Dereva wa gari hilo lililokuwa likiendeshwa kwa kasi anasemekana kurusha nje magunia matatu yaliyokuwa na bidhaa hiyo alipogundua kuwa alikuwa akifuatwa na kutoweka.

Maafisa wa usalama waliyatwaa magunia hayo yaliyokuwa na misokoto ya bangi na kuyapeleka katika kituo cha polisi cha Molo kwa uchunguzi.

Kutokana na operesheni hiyo afisa mkuu mtendaji wa NACADA Anthony Omerikwa amepongeza umma kwa kutoa taarifa iliyopelekea kunaswa kwa dawa hizo za kulevya.

‘‘Operesheni hii inaashiria jukumu muhimu la wananchi katika kusaidia jitihada za utekelezaji wa sheria,’’ alisema huku akisisitiza kujitolea kwa mamalaka ya NACADA kuendeleza operesheni ya kitaifa dhidi ya dawa za kulevya.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here