Serikali ya Kenya imeahidi kwamba itakuwa ikimtuza shilingi milioni tano mwanariadha yeyote anayeandikisha rekodi mpya katika mashindano ya kimataifa.
Katika hafla ya kumzawadi mshikilizi wa rekodi ya mbio za mita elfu tano na elfu moja mia tano upande wa wanawake Faith Kipyegon katika ikulu, rais William Ruto amesema hii ni njia moja ya kuwachochea wanariadha kuandakisha matokeo bora.
Kiongozi wa taifa amemtuza Kipyegon kima cha shilingi milioni tano pamoja na nyumba yenye dhamani ya shilingi milioni sita kwa kuvunja rekodi mbili za dunia katika mashindano ya mbio za mita elfu tano na elfu moja mia tano mtawalia.
Aidha rais ameamuru idara ya uhamiaji kuwapa pasipoti ya kidiplomasia wanariadha wanaotia fora.
“Nataka pia kuuliza wizara inayohusika na mambo ya uhamiaji kuhakikisha kwamba wanariadha wetu wanaofanya vyema wanapewa pasipoti za kidiplomasia pamoja na tuzo za kitaifa.” alisema rais.
Mwanariadha huyo aliandikisha rekodi mpya ya dakika 3:49:1 kwenye mbio za mita elfu moja mia tano zilizofanyika nchini Italia na kuwa mwanamke wa kwanza ulimwenguni kumaliza mbio hizo chini ya muda wa dakika 3:50 kabla ya kuandikisha rekodi nyingine katika mbio za mita elfu tano wiki moja baadaye katika taifa la Ufaransa
Akipokea zawadi hiyo bingwa huyo mpya wa dunia hakuficha furaha yake na kushukuru serikali ya Kenya kutambua juhudi za wanariadha.
“Nimefurahia sana, sijui nianzie wapi? nimalizie wapi?, nina hisi furaha kuwa hapa, nahisi serikali imetambua juhudi zangu baada ya kurejea nyumbani na kupokelewa kwa njia hii inaridhisha moyo wangu” alisema Kipyegon.
Serikali aidha imeweza kumtuza shilingi milioni mbili bingwa wa Afrika katika mbio za mita mia moja Ferdinand Omanyala baada ya kumaliza wa pili katika mashindano ya riadha yaliyofanyika nchini Italia.