Mbunge wa Juja, George Koimburi, ameachiliwa kwa dhamana ya Shilingi 100,000 pesa taslimu na Mahakama Milimani siku ya Jumatatu, baada ya kukana mashtaka manne ya ulaghai katika kesi ya ardhi ya thamani ya Shilingi milioni 10.
Koimburi, pamoja na Shelmith Karungri Maina na Gathi Irungu, wanatuhumiwa kwa kula njama ya kumlaghai mfanyabiashara Julius Gitonga kipande cha ardhi chenye ukubwa wa ekari 1.3 kilichoko Ruiru, Juja mashariki.
Wakati wa kutajwa kwa kesi hiyo mbele ya hakimu mkuu Robinson Ondieki, wakili wa Koimburi aliomba mahakama imwachilie bila dhamana, akidai kuwa mlalamishi alikuwa amefika mahakamani na kuonyesha nia ya kuondoa kesi hiyo ombi lililopingwa na upande wa mashtaka.
”Mlalamishi tayari ameonyesha nia ya kuondoa kesi hii. Mteja wangu kwa hivyo hana uwezekano wa kutoweka na anastahili kuachiliwa bila dhamana’’ wakili wake alieleza mahakama.
Katika kesi hiyo Maina ambaye ni mshtakiwa wa pili tayari yuko nje kwa dhamana ya shilingi sh 100, 000 huku wa tatu akisemekana kuwa nje ya nchi kwa sababu za kimatibabu.
Kesi hiyo imeratibiwa kutajwa tarehe 22 mwezi Oktoba.









