Huenda Wakenya hivi karibuni wakapata huduma mbalimbali za serikali katika Kituo cha Huduma kilicho karibu nao kufuatia agizo jipya linaloyataka mashirika kutoa huduma zote zinazowalenga raia katika vituo hivyo.
Akizungumza katika Ukumbi wa Kimataifa wa Mikutano wa Kenyatta (KICC) wakati wa maadhimisho ya Wiki ya Utumishi wa Umma Jumanne, Juni 23, 2026, Waziri wa Utumishi wa Umma Geoffrey Ruku ameagiza wizara, idara na mashirika yote ya serikali kuhakikisha huduma zote zinazotolewa moja kwa moja kwa umma zinapatikana kupitia Vituo 59 vya Huduma nchini.
Ameongeza kuwa agizo hilo limetoka kwa Rais William Ruto katika juhudi za kuboresha utoaji wa huduma na uzoefu wa wateja katika sekta ya umma.
“Tumeagiza wizara, idara na mashirika yote ambayo yana huduma zinazowalenga raia, huduma hizo zote lazima zipatikane katika Vituo vya Huduma,” amesema.
Kwa sasa, Huduma Kenya inatoa huduma 165 kutoka wizara, idara na mashirika 51 pamoja na serikali 35 za kaunti.
Hata hivyo, kulingana na Afisa Mkuu Mtendaji wa Huduma Kenya Benjamin Kai, ni mashirika 11 pekee ya serikali ya kitaifa ambayo yamesambaza huduma katika Vituo vyote vya Huduma kote nchini.









