Rais Uhuru Kenyatta anasubiri kumteua rasmi Martha Karambu Koome kuwa Jaji Mkuu mpya baada ya kuwashinda wawaniaji wengine 10 waliohojiwa kwa wadhifa huo.
Tume ya huduma za mahakama (JSC) chini ya uenyekiti wake Profesa Olive Mugenda imetangaza kuwa jaji Koome aliibuka bora kufuatia mahojiano yaliyokamilika juma lililopita.
Iwapo atateuliwa na rais baada ya kuidhinishwa na bunge, jaji Koome atakuwa mwanamke wa kwanza nchini kushikilia wadhifa huo.
Jaji Koome ni mzaliwa wa mwaka 1960 kaunti ya Meru na ana uzoefu wa miaka 33 katika maswala ya kisheria tangu mwaka 1987.
Koome alijiunga na idara ya mahakama mwaka 2003 ambapo amekuwa akipanda ngazi kutoka mahakama kuu hadi mahakama ya rufaa.
Waliohojiwa kumrithi David Maraga aliyestaafu ni rais wa mahakama ya rufaa William Ouko, Juma Chitembwe, David Marete, mawakili Fred Ngatia na Philip Murgor pamoja na wasomi wa maswala ya kisheria Profesa Kameri Mbote na Dr. Dr. Moni Wekesa.