Mahakama yawazuilia polisi wanaoshutumiwa kumpiga risasi mchuuzi

0

Mahakama imeagiza maafisa wawili wa polisi wanaotuhumiwa kwa kumfyatulia risasi mchuuzi wa barakoa Boniface Mwangi Kariuki wakati wa maandamano ya Jumanne, tarehe 17 Juni 2025 jijini Nairobi wazuiliwe kwa siku kumi na tano uchunguzi dhidi yao ukiendelezwa.

Katika agizo lililotolewa Alhamisi 19 Juni 2025, hakimu mkuu wa mahakama ya Milimani BenMark Ekhubi aliagiza kuzuiliwa kwa konstebo Klinzy Barasa Masinde na Duncan Kiprono katika kituo cha polisi cha Capitol Hill jijini Nairobi hadi tarehe 3 Julai 2025 watakapowasilishwa tena mahakamani.

Upande wa mashtaka ukiongozwa na mamlaka huru ya kuangazia utendakazi wa maafisa wa polisi (IPOA) ulikuwa umeomba muda wa siku ishirini na moja zaidi kuwazuilia wawili hao ili kutoa muda kwa maafisa wa idara ya upelelezi (DCI) kuendeleza uchunguzi kwa hofu ya uwezekano wa kuhitilafiwa kwa ushahidi iwapo wangeachiliwa kwa dhamana.

Wahusika wanashutumiwa kumpiga Kariuki risasi kichwani na kumsababishia majeraha mabaya, tukio ambalo lilinaswa kwenye video iliyosambazwa kwenye mitandao ya kijamii na kuzua hisia kutoka kwa umma pamoja na makundi mbalimbali ya kiraia.

Kulingana na stakabadhi zilizowasilishwa mahakamani Kariuki alikuwa akiendelea kupokea matibabu katika hospitali ya kitaifa ya Kenyatta (KNH) akiwa katika chumba cha wagonjwa mahututi baada ya kufanyiwa upasuaji.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here