Mahakama ya rufaa imefungua njia ya utekelezaji wa mfumo wa ushirikiano wa afya kati ya Kenya na Marekani, kwa kuondoa amri za mahakama kuu zilizokuwa zimezuia mpango huo.
Jopo la majaji watatu limebatilisha amri za muda zilizotolewa tarehe 19 Desemba 2025, likiamua kuwa maslahi ya umma katika kuendeleza huduma muhimu za afya yana uzito mkubwa kuliko hatari zinazoweza kutokea kwa kuruhusu mpango huo kuendelea kabla ya mzozo wa kisheria kutatuliwa.
Majaji hao walionya kuwa kuendelea kusimamishwa kwa utekelezaji wa mfumo huo kunaweza kuvuruga huduma muhimu za afya, zikiwemo matibabu ya HIV, kifua kikuu (TB), Malaria na magonjwa mengine ya kuambukiza, pamoja na programu za chanjo.
“Maisha ya wananchi wanaotegemea matibabu ya HIV, TB na Malaria yanayotolewa chini ya mfumo huu yako katika hatari ya kuathiriwa vibaya na kwa namna isiyoweza kurekebishwa,” majaji hao waliamua.
Mfumo huo ulitiwa saini na Kenya na Marekani tarehe 4 Desemba 2025, na unahusishwa na utoaji wa dawa muhimu, msaada wa huduma za afya na huduma nyingine zinazotegemewa na mamilioni ya wakenya.
Serikali, kupitia mwanasheria mkuu na waziri wa Afya, ilikuwa imewasilisha ombi la kusimamisha utekelezaji wa amri za mahakama kuu wakati ikisubiri kusikilizwa na kuamuliwa kwa rufaa iliyokusudia kuwasilisha.
Katika ombi lake, serikali ilionya kuwa kuzuia makubaliano hayo kunatishia programu za afya zinazohudumia takriban wakenya milioni 1.4.
Mahakama ya rufaa ilikubaliana kuwa matokeo ya kuendelea kusimamishwa kwa mpango huo yanaweza kuwa yasiyoweza kurekebishwa, hasa ikiwa rasilimali zilizotengewa programu hiyo zitaelekezwa kwenye matumizi mengine kabla ya rufaa kuamuliwa.
Uamuzi huo ulifuatia upinzani kutoka kwa mwanaharakati wa masuala ya kikatiba, Okiya Omtatah Okoiti, ambaye alidai kuwa kuruhusu mfumo huo kuendelea kabla ya changamoto ya kikatiba kutatuliwa kunaweza kudhoofisha haki za msingi na uwajibikaji wa umma.
Omtatah alieleza wasiwasi kuhusu ulinzi wa data, fedha za umma, ugatuzi wa madaraka na nafasi ya bunge katika kuidhinisha makubaliano ya kimataifa yanayoweka wajibu wa kisheria na ahadi za kifedha kwa Kenya.
Shirika la Katiba Institute pia lilipinga ombi la serikali, likisisitiza kuwa kinga za kikatiba na usimamizi wa bunge havipaswi kupuuzwa kwa kisingizio cha kuharakisha utoaji wa huduma za afya.
Mahakama ilifafanua kuwa uamuzi wake haukutatua mgogoro mkuu kuhusu uhalali wa makubaliano hayo kikatiba, bali ulihusu suala la iwapo amri zilizozuia utekelezaji wake zinapaswa kuendelea kutumika wakati wa kusubiri rufaa.
Uamuzi huo unaipa serikali nafasi ya kuendelea na mpango wa ushirikiano wa afya huku changamoto pana ya kisheria ikiendelea kushughulikiwa mahakamani.









