Mahakama Kuu imetangaza Kifungu cha 29(c) cha Sheria ya urithi kuwa kinyume na katiba, ikitaja ubaguzi wa kijinsia dhidi ya wajane kina baba.
Jaji Lawrence Mugambi ameamua kwamba kifungu hicho—ambacho kinamtaka mume kuthibitisha kwamba anamtegemea mke wake aliyefariki ili kuwa mrithi wa mali yake—kinakiuka haki ya usawa na kutobaguliwa.
Kesi hiyo iliwasilishwa na mume wa marehemu Caroline Wawira Njagi.
Kwenye uamuzi huo, jaji Mugambi amesema ni ubaguzi wa kijinsia kwa mwanamme kuhitajika kudhihirisha alikuwa anamtegemea mke wake ilhali sio vile kwa wake wanaowapoteza waume wao.
Inaarifiwa mlalamishi na marehemu walikuwa wameoana chini ya Sheria ya Kimila ya Kiembu tangu 2002 na kujaliwa watoto wawili kabla ya kutengana 2022, huku wakidumisha uhusiano mzuri na kulea watoto wao kwa pamoja.
Kufuatia kifo cha Wawira mnamo Julai 2023, mlalamishi hakujumuishwa katika mipango ya mazishi na mwenzi wa marehemu, na kusababisha mabishano ya kisheria ambayo hatimaye yalimpa haki ya mazishi kupitia Mahakama ya Mavoko.
Kifungu cha 29(c) cha Sheria ya urithi kinahitaji mwanamme mjane kudhibitisha alikuwa akimtegemea mke wake kabla ya kuaga kwake.









