Jane Muthoni aliyepatikana na hatia ya kumuuaa mumewe miaka minne iliyopita amehukumwa kifungo cha miaka thelathini gerezani.
Katika hukumu hiyo iliyotolewa na Jaji Joel Ngugi wa mahakama ya Nakuru, Muthoni atatumikia kifungo chake kuanzia Novemba mwaka 2016 wakati alikamatwa na kuzuiliwa.
Mshukiwa mwenza Isaac Nganga, almaarufu Gikuyu pia amehukumiwa kifungo cha miaka 30 na atatumikia kuanzia Disemba mwaka 2016.
Muthoni ambaye ni mwalimu mkuu wa zamani ya shule ya wasichana ya Icaciri alipatikana na hatia ya kumlipa Nganga na mshukiwa mwingine Nelson Njiru aliyetoroka kumuua mumewe Solomon Mwangi ambaye ni mwalimu mkuu wa zamani wa shule ya wavulana ya Kiiru kaunti ya Muranga Novemba mwaka 2016.
Muthoni alimtuhumu mumewe kwa kuwa na uhusiano wa nje ya ndoa huku uchunguzi ukibaini kuwa washukiwa walipanga kumuua mwanamke aliyedaiwa kuwa na uhusiano na Mwangi.
Mwili wa Mwangi ulipatiakana mapema mwezi Novemba mwaka 2016 katika shamba la kahawa la Karakuta, eneo la Juja kaunti ya Kiambu.
Hukumu hiyo imetolewa licha ya wanawe kuiomba mahakama kumuachilia mama yao kutokana na hali ngumu wanayopitia.