Jaji Martha Koome kuhojiwa kwa wadhifa wa jaji mkuu

0

Hii leo (Jumatano) ni zamu ya jaji wa mahakama ya rufaa Martha Koome kufika mbele ya tume ya huduma za mahakama (JSC) kuhojiwa kwa wadhifa wa jaji mkuu.

Jaji Koome ni mzaliwa wa mwaka 1960 kaunti ya Meru na ana uzoefu wa miaka 33 katika maswala ya kisheria tangu mwaka 1987.

Koome atakayekuwa mwanamke wa pili kuhojiwa kwa wadhifa huo alijiunga na idara ya mahakama mwaka 2003 ambapo amekuwa akipanda ngazi kutoka mahakama kuu hadi mahakama ya rufaa.

Jaji Koome anahojiwa siku moja baada ya Profesa Patricia Kameri Mbote kunadi sera zake mbele ya JSC kwa kueleza kuwa atatumia uzoefu wake katika maswala ya kisheria kuboresha utendakazi wa idara ya mahakama iwapo atateuliwa kuwa jaji mkuu.

Ameahidi kutathmini mabadiliko yaliyoanzishwa na watangulizi wake Dkt. Willy Mutunga na David Maraga kufahamu yalikofikia kwa makusudi ya kujua ni vipi wataimarisha zaidi utendakazi wa mahakama.

Kuhusu madai ya kuwepo kwa ufisadi katika idara ya mahakama, Profesa Mbote ameelezea kuwepo kwa haja ya kushughulikia tatizo hilo ndani kwa ndani ili kuondoa dhana hiyo kwa umma.

Jaji wa mahakama kuu Said Juma Chitembwe alifungua ukurasa wa mahojiano hayo akisema ana uwezo wa kumrithi David Maraga aliyestaafu kwa sababu ya uzoefu wake katika idara ya mahakama.

Watu 10 wameorodheshwa kuhojiwa kwa wadhifa huo.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here