Beki wa timu ya taifa ya kandanda (Harambee Stars), Collins Sichenje, anatazamia kuwaridhisha mashabiki wa klabu yake ya Charlton Athletic ya Uingereza itakapokabiliana na Tottenham Hotspur katika mechi ya kombe la Carabao Jumatano usiku.
Mchezaji huyo mkenya mwenye umri wa miaka 22 amesema anafurahia changamoto ya kucheza ugenini katika uwanja wa Tottenham Hotspur jijini North London nchini Uingereza, licha ya uchache wa mashabiki wa Charlton maaurufu ‘The Addicks’ ikilinganishwa na mashabiki wa timu ya nyumbani.
“Mashabiki wote wa Charlton ni wazuri sana na walifanya kazi nzuri katika mechi dhidi ya West Ham, kwani uliweza kuwasikia wakishangilia kwa sauti kubwa mbele ya mashabiki 60,000. Haijalishi watakuja wangapi, sisi tutatumia nguvu zao na kuwapigania kwa sababu wanastahili,” alisema Sichenje.
Beki huyo wa kati huenda akaanza katika kikosi cha Nathan Jones kwa mechi hiyo, baada ya kupata muda mchache wa kucheza msimu huu wa 2026/27.
Alishiriki kwa dakika sita katika mechi yao ya kwanza ya Championship ya Uingereza, wa ushindi wa 2-1 dhidi ya Derby, kabla ya kucheza dakika nyingine 14 katika ushindi wa 2-1 dhidi ya West Ham wikendi iliyopita.
Wakati Sichenje akiwa na hamu kubwa ya kupata dakika zaidi uwanjani, mkenya mwenzake Timothy Ouma bado yuko nje ya kikosi cha kwanza.
Kiungo huyo wa zamani wa Nairobi City Stars alijiunga na Charlton wiki mbili zilizopita kwa mkopo kutoka kwa vigogo wa Jamhuri ya Czech, Slavia Prague.
Ouma bado hajacheza mechi yoyote huku akiendelea kujenga utimamu wake wa mwili nje ya uwanja na kujitahidi kwa bidii kupata nafasi katika kikosi cha siku ya mechi.









