Mahojiano ya kuwatafuta makamishna wapya wa tume huru ya uchaguzi na mipaka nchini (IEBC) yamekamilika rasmi baada ya majuma mawili ya kuwasaili zaidi ya watu 30.
Kibarua sasa ni kwa jopo la uteuzi chini ya uenyekiti wake Dr. Elizabeth Muli kutathmini waliohojiwa na kupendekeza kwa rais Uhuru Kenyatta majina ya watu wanne watakaojaza nafasi hizo.
Mahojiano hayo yamekamilika kwa kuhojiwa kwa watu watatu Ijumaa ambao ni Roseline Odede, Rose Musyoka na Profesa Richard Oduor.
Profesa Oduor amekabiliwa na kibarua kujibu baadhi ya maswali ikiwemo majina ya makamishna wa sasa wa tume ya IEBC.
Kwa upande wake, aliyekuwa kamishna wa tume ya ardhi nchini Dr. Musyoka amekabiliwa na kibarua cha ziada kuelezea utendakazi wake akiwa kwa tume ya ardhi nchini.
Watakaoteuliwa watachukua nafasi za Rosyline Akombe, Connie Maina, Margret Mwachanya na Paul Kurgat waliojiuzulu.









