Gavana wa Wajir Ahmed Abdullahi amechaguliwa kuhudumu kwa kipindi cha pili akiwa mwenyekiti wa baraza la magavana nchini (COG).
Katika uchaguzi wa viongozi wa kamati tendaji na kiufundi wa baraza hilo uliofanyika Jumatatu tarehe 6 Oktoba jijini Nairobi, gavana wa Nyeri Mutahi Kahiga sawia alichaguliwa kwa mara ya pili kuwa naibu mwenyekiti.
Gavana wa kaunti ya Tharaka Nithi Muthomi Njuki ambaye awali aliongoza kamati ya Afya, alichaguliwa kuwa kiranja wa baraza hilo nafasi iliyoshikiliwa awali na Stephen Sang wa Nandi huku gavana wa Mombasa Abdulswamad Shariff Nassir akimrithi katika kamati ya Afya.
Mbali na hao pia magavana mbalimbali walichaguliwa kuongoza kamati tofauti za baraza hilo kwa kipindi cha mwaka mmoja.
Magavana kupitia mwenyekiti wao mpya waliwahakikishia wakenya kujitolea kwao kuimarisha jukumu la baraza hilo kulinda ugatuzi.
‘‘Sisi tuliochaguliwa kutoa huduma tunajitolea kuzingatia masuala yaliyo kipaumbele katika kuimarisha jukumu la baraza na kulinda ugatuzi,’’ Abdullahi alisema.
‘‘Masuala hayo ni pamoja na kuendesha taasisi ya mafunzo ya ugatuzi, kutekeleza mpango mkakati wa 2022-2027.’’
Wakati huo huo magavana walisema kuwa huduma za ununuzi na uagizaji zinaendelea vyema katika kaunti zote kufuatia amri ya mahakama iliyozuia agizo la hazina ya kitaifa lililotaka shughuli zote za ununuzi na uagizaji kufanywa kupitia njia ya kidijitali.