WATALII WAAGA DUNIA WAKIWA SAFARINI KUTOKA MASAI MARA

0

Watalii watano wenye asili ya Kihindi wamethibitishwa kuaga dunia huku wengine kadhaa wakijeruhiwa katika ajali ya barabarani iliyotokea katika kijiji cha Gichaka, kwenye barabara ya Nakuru-Ol Joro Orok, Kaunti ya Nyandarua.

Inaripotiwa kuwa watalii hao walikuwa wakisafiri kutoka Hifadhi ya Masai Mara kuelekea Nyahururu kwa basi dogo (matatu ya watalii) lililopata hitilafu ya breki walipokuwa wakishuka mlima kuelekea eneo la Ol Joro Orok.

Basi hilo lilianguka kwenye mtaro baada ya dereva, ambaye ni miongoni mwa walionusurika, kujaribu kulikata kona karibu na Shule ya Uhuru Comprehensive katika eneo la Gichaka.

Gari hilo lilipinduka mara kadhaa kabla ya kutua katika shamba la viazi, paa lake likiwa limechanika kabisa kutokana na athari za ajali hiyo.

Akidhibitisha ajali hiyo, Kamanda wa Polisi wa Kaunti ya Nyandarua, Stella Cherono, amethibitisha kuwa watu watano walifariki papo hapo, huku manusura wengine wakikimbizwa katika Hospitali ya Rufaa ya Kaunti ya Nyahururu, Hospitali ya St.Benedict huko Nyahururu na pia katika jiji la Nakuru.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here