Serikali imekuwa ikikopa wastani wa shilingi bilioni 5.9 kila wiki kwa kipindi cha miezi minne iliyopita.
Hii ni kulingana na takwimu mpya iliyotolewa na hazina ya kitaifa ishara ya kuongezeka kwa utegemezi wa madeni kufadhili shughuli zake za kila siku.
Ripoti hiyo inayohusu kipindi cha kuanzia Mei Mosi hadi Agosti 30 2025 inaonyesha kwamba jumla ya shilingi bilioni 95.5 zilikopwa katika kipindi hicho kutokana na ongezeko la nakisi ya bajeti na ucheleweshaji wa ukusanyaji wa mapato ya serikali.
Kulingana na nyaraka zilizowasilishwa bungeni Jumanne, Oktoba 7, 2025 fedha hizo zilipatikana kutokana na ukopeshaji wa kimataifa, washirika wa maendeleo na taasisi za kibiashara zikilenga kufadhili miradi mbalimbali humu nchini.
Kwa mujibu wa takwimu, Kenya imekuwa ikikopa takriban shilingi bilioni 23.9 kila mwezi ambazo ni sawa na shilingi milioni 795 kila siku na shilingi milioni 532.4 kila saa.
Ripoti hiyo imeibua wasiwasi baada ya kubainika kuwa taifa limevuka kiwango cha juu cha kisheria cha madeni huku wanauchumi na wabunge wakionya kwamba hali hiyo inaweza kuweka uchumi katika hatari kubwa ya kushindwa kulipa madeni na kuathiri miradi ya maendeleo.
Waziri wa fedha John Mbadi alisema kufikia Juni mwaka 2025 deni la taifa lilifikia shilingi trilioni 11.81 sawa na asilima 67.8 ya pato la jumla (GDP) likiwa juu Zaidi za kiwango cha kisheria cha asilimia 55 kilichowekwa na bunge.