RUTO, RAILA WABUNI TIMU YA WANACHAMA 5 KUTEKELEZA AJENDA 10, RIPOTI YA NADCO

0

Rais William Ruto na kinara wa chama cha ODM Raila Odinga wamebuni kamati ya watu watano itakayosimamia utekelezaji wa Ajenda yenye vipengele 10 na Ripoti ya NADCO.

Hii ni sehemu ya Mkataba wa Maelewano (MoU) baina ya viongozi hao wawili ya Machi 7, 2025.

Makubaliano kati ya Muungano wa UDA na chama cha ODM yanalenga kukuza uwiano wa kitaifa na kuendeleza ustawi jumuishi kupitia kile viongozi hao wawili walichoeleza kama mfumo mpana wa ushirikiano kati ya makundi yote ya kisiasa na washikadau wengine wakuu.

Kulingana na taarifa ahadi za Mkataba wa Maelewano ni pamoja na utekelezaji kamili wa Ripoti ya NADCO, ushirikishwaji katika maisha ya umma, ulinzi na uimarishaji wa ugatuzi, kulinda maisha ya vijana na kukuza uongozi na uadilifu.

Pia italenga kuhakikisha haki ya kukusanyika kwa amani, kushughulikia deni la taifa, kupambana na rushwa, kuzuia upotevu wa rasilimali za umma, na kulinda na kukuza mamlaka ya watu, utawala wa sheria, na Katiba.

Kamati hiyo itaongozwa na Agnes Zani, huku Fatuma Ibrahim, Kevin Kiarie, Gabriel Oguda, na Javas Bigambo wakiwa wanachama.

 

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here