Tume ya IEBC Yaatoza faini wagombea wa Kasipul Boyd Were na Philip Aroko ya shilingi Milioni Moja

0

Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka nchini (IEBC) imewatoza faini ya Shilingi milioni moja wagombeaji wa kiti cha ubunge wa Kasipul Boyd Were na Philip Aroko kila mmoja kufuatia ghasia za hivi majuzi zilizoshuhudiwa katika eneo bunge hilo wakati wa kampeni.

Wakihutubia wanahabari Kamati ya Utekelezaji ya Maadili ya Uchaguzi ya IEBC imewaamuru wagombeaji hao wawili walipe faini hiyo ndani ya saa 48 la sivyo wachukuliwe hatua zaidi za kinidhamu.

“Philip Aroko anatakiwa kulipa faini ya Ksh1 milioni kwa IEBC ndani ya saa 48, vile vile, Boyd Were pia anatakiwa kulipa Ksh1 milioni kwa IEBC ndani ya saa 48 za maagizo haya,” IEBC imesema.

IEBC aidha imeonya kwamba iwapo wagombeaji wowote kati ya hao wawili watarudia makosa yoyote ya uchaguzi kama ilivyoshuhudiwa wakati wa kampeni za hivi majuzi katika eneo bunge hilo, basi watazuiwa kushiriki katika uchaguzi huo.

“Onyo kali zaidi linatolewa kwa wagombea wote wawili kwamba endapo watahusishwa na visa sawia na vya awali kamati hii itazingatia adhabu zote chini ya sheria, ikiwa ni pamoja na kuzuiliwa kushiriki uchaguzi mdogo,” Tume iliongeza.

Kando na kuwatoza faini wagombea hao wawili, Kamati pia iliagiza wagombeaji wote wa uchaguzi mdogo wa eneobunge la Kasipul kutii kikamilifu ratiba ya kampeni iliyowianishwa na kukubaliwa.

IEBC pia imefichua kuwa imepokea ripoti za kijasusi zinazohusisha Serikali ya Kaunti ya Homa Bay moja kwa moja na kampeni za uchaguzi mdogo wa Kasipul.

Tume hiyo imekosoa utawala wa Gavana Gladys Wanga, ikiushutumu kwa madai ya kutumia vibaya rasilimali za umma kuingilia masuala ya kisiasa ya Kasipul kinyume na sheria.

“Kamati hii inalaani matumizi ya rasilimali za umma na kuhusika kwa maafisa wa umma katika kampeni za kisiasa, kwani hii ni kinyume na Kifungu cha 14 cha Sheria ya Makosa ya Uchaguzi,” IEBC ilithibitisha.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here