Muungano wa Wamiliki wa Matatu (MOA) umetishia kuitisha mgomo wa kitaifa Jumatatu, tarehe 2 Februari, endapo serikali haitachukua hatua kukabili ongezeko la visa vya matatu kuchomwa moto.
Uamuzi huo umefikiwa kufuatia mfululizo wa matukio ambapo matatu zinadaiwa kuchomwa moto na waendeshaji wa bodaboda.
Katika mahojiano ya kipekee na Shajara, Mwenyekiti wa MOA Albert Karakacha alisema kuwa matukio hayo yameripotiwa kwa polisi na barua kuandikwa kwa Wizara ya Uchukuzi, lakini hakuna hatua iliyochukuliwa hadi sasa.
“Malalamishi yetu makuu ni kuchomwa kwa mabasi yetu na waendeshaji wa bodaboda. Tumeripoti matukio haya kwa polisi na pia tumeandika barua kwa Wizara ya Uchukuzi lakini hakuna hatua iliyochukuliwa. Haya yamekuwa yakitokea kote nchini. Kwa hivyo, tutasitisha huduma zetu hadi hatua ichukuliwe,” alisema Karakacha.
Karakacha alisema kuwa wanashirikiana na Chama cha Madereva Binafsi nchini (Motorists Association) katika hatua hiyo, akiongeza kuwa wamiliki wa matatu hupata hasara kubwa magari yao yanapochomwa moto. Wametaka wahusika wa uhalifu huo wakamatwe na kuadhibiwa sheria.
Kwa upande wao, Chama cha Madereva Binafsi nchini Kenya (MAK) kilisema kuwa kwa niaba ya wafanyakazi wa sekta ya uchukuzi, wamiliki wa magari binafsi, wasafirishaji na madereva wa malori, watasitisha shughuli zao ili kuwaunga mkono waendeshaji wa matatu, wakitaja visa vya mara kwa mara vya magari kuchomwa moto na kile walichosema ni ukosefu wa mwitikio kutoka kwa serikali.
Haya yanajiri siku chache baada ya matatu ya Forward Travelers Sacco kuchomwa moto, baada ya dereva kudaiwa kugonga mwendeshaji wa bodaboda na kujaribu kutoroka eneo la tukio kwenye barabara ya Juja, Nairobi.









