FAMILIA ZA WALIOPIGWA RISASI KASARANI ZALILIA HAKI

0
Babake Vincent Otieno, Meshack Ogutu (Kulia) na Yvonne Akinyi, mkewe Vincent (katikati)

Wakiwa bado wanakumbwa na mshtuko na huzuni kufuatia kifo cha Waziri Mkuu wa zamani Raila Amolo Odinga, waombolezaji walifurika katika Uwanja wa Michezo wa Kimataifa wa Moi-Kasarani siku ya Alhamisi, Oktoba 16, 2025, kwa ajili ya kuutazama mwili wake.

Hata hivyo, vurugu zilizuka uwanjani humo na polisi walidaiwa kufyatua risasi dhidi ya waombolezaji, ambapo watu watatu walipoteza maisha yao. Waathiriwa – wote wakiwa raia wasio na silaha – walidaiwa kupigwa risasi na maafisa wa polisi katika kile mashirika ya haki za binadamu yameelezea kama mauaji ya kikatili.

Kulingana na matokeo ya uchunguzi wa maiti yaliyotolewa Jumanne, Oktoba 21, 2025 katika makafani ya Nairobi, Evans Kiche mwenye umri wa miaka 36, baba wa watoto watatu, alikufa kutokana na risasi moja kichwani iliyovunja fuvu na kuharibu ubongo wake. Ndugu yake mwenye huzuni, Gilbert Okeyo, alilaani mauaji hayo na kuhoji hatua za polisi.
“Kwa nini polisi walitumia risasi kwa waombolezaji ilhali wangeweza kutumia mbinu salama zaidi?”

Binamu yake Kiche, Moses Kaumba, alimtaja marehemu kama mtu wa amani ambaye alikuwa ameenda Kasarani “kumlilia shujaa wake, Raila Amolo Odinga,” akiongeza kuwa kifo chake kilikuwa cha kikatili na kisicho na maana.
Kaumba alithibitisha kuwa marehemu atazikwa nyumbani kwake Kanjira, katika eneo bunge la Karachuonyo, Kaunti ya Homa Bay mnamo Novemba 10, 2025.

Mwathiriwa mwingine, Vincent Otieno Ogutu mwenye umri wa miaka 35, alifariki kutokana na jeraha la risasi kifuani lililopenya hadi moyoni. Kipande cha risasi kilipatikana mwilini mwake. Mkwe wake, Paul Nyalo, alisema risasi hiyo ilikuwa na nia ya kumuua.
“Ukiangalia alipopigwa risasi, ni wazi Vincent alipigwa risasi kwa madhumuni ya kumaliza maisha yake,” Nyalo alilalamika.

Baba yake, Meshack Ogutu Okode, na mjane wake, Yvonne Akinyi Empire, wametoa wito wa haki na kudai serikali kutoa majibu kuhusu kifo hicho cha kusikitisha, wakisema ameachwa kulea watoto watatu wadogo peke yake.
“Na haki itendeke kwa mume wangu,” aliomba kwa machozi.

Mwadhiriwa wa tatu, Jidah Burka, alithibitishwa kufariki kutokana na risasi moja kichwani. Risasi iliingia kutoka mbele na kutokea nyuma ya kichwa na kumuua papo hapo. Mwili wake umeachiliwa kwa familia yake na mazishi yalifanyika katika makaburi ya Waislamu ya Kariokor.

Mamlaka Huru ya Uangalizi wa Polisi (IPOA) imeanza uchunguzi kuhusu mauaji hayo.
Mtetezi wa haki za binadamu, Hussein Khalid, alilaani vikali tukio hilo akilielezea kama ishara ya “utendaji kazi wa polisi wenye pupa ya bastola,” na akishutumu kikosi maalum ndani ya huduma ya polisi kwa kuwalenga raia.
“Hii si polisi -haya ni mauaji… Polisi lazima wapate njia za kudumisha utulivu wa umma bila kuua watu wasio na hatia na wasio na silaha,” alisema Khalid.

Ufyatuaji risasi wa polisi wa hivi karibuni huko Kasarani umechochea zaidi tatizo sugu la kitaifa la ukatili wa polisi na pia umeibua wito wa uwajibikaji na mjadala mpya kuhusu matumizi ya nguvu kupita kiasi na polisi nchini Kenya, huku familia za waombolezaji waliouawa zikidai jambo moja –Haki!

 

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here