Mahakama ya Shanzu jijini Mombasa imeamuru kuzuiliwa kwa siku 30 washukiwa sita wa ulanguzi wa dawa za kulevya zenye dhamani ya shilingi bilioni 8.
Hii ni baada ya hakimu mkuu Antony Mwicigi Jumanne 27 Oktoba 2025 kukubali ombi la mkurugenzi wa mashtaka ya umma DPP la kuwazuilia raia hao wa kigeni ili kukamilisha uchunguzi.
Sita hao wenye uraia wa Iran walikamatwa Jumamosi 24 Oktoba 2025 wakihusishwa na shehena iliyokuwa na dawa za kulevya zilizokadiriwa kuwa zenye dhamani ya shilingi bilioni nane.
Mwicigi katika uamuzi wake aliamuru kuwa washukiwa hao wasalie kizuizini katika kituo cha polisi cha Bandari uchunguzi dhidi yao ukiendelezwa kabla ya mwelekeo zaidi kutolewa.
Vilevile mahakama iliamuru wapelelezi katika kesi hiyo kuwasilisha bidhaa iliyonaswa kwenye maabara ya serikali pamoja na simu za washukiwa kwa uchunguzi katika makao makuu ya Idara ya upelelezi (DCI).
Katika mawasilisho yake mahakamani, afisa wa upelelezi katika kesi hiyo alieleza kwamba washukiwa walitiwa mbaroni tarehe 24 Octoba 2025 wakiwa wameabiri meli iliyofumaniwa na maafisa wa jeshi la wanamaji katika bandari ya Kilindini akieleza kuwa walikuwa wakichunguzwa kwa uwezekano wa kushiriki ulanguzi wa dawa za kulevya kinyume na sheria.
Jumla ya vifurushi 769 vyenye uzito wa kilo 1,035 vilivyokuwa na bidhaa iliyoshukiwa kuwa dawa za kulevya vilinaswa wakati wa tukio
Kesi hiyo iliratibiwa kutajwa tarehe 14 Novemba 2025.









