Maaskofu wa kanisa la Africa Inland Church (AIC) nchini Kenya, chini ya mwavuli wa baraza kuu wametoa wito kwa wakenya kushirikiana na serikali tawala katika utekelezaji wake wa miradi ya maendeleo ili kuchochea ufanisi wa taifa.
Wakiongozwa na askofu mkuu wa kanisa hilo nchini Kenya Abraham Mulwa aliyezungumza baada ya mkutano wao wa baraza kuu uliofanyika jijini Nairobi siku ya Alhamisi tarehe 23 Oktoba, waliwataka wakenya kudumisha amani wakidokeza kwamba kama viongozi wa makanisa wanazidi kuliombea taifa.
‘‘Na tunawatakia wakenya mema, tunaomba na kuwarai wakenya wote kudumisha amani na kuunga serikali katika kuafikia malengo yake,’’ alisihi askofu Mulwa.
‘‘Tunamwombea rais wetu, baraza la mawaziri na wananchi wa jamuhuri ya Kenya, tunawasihi wakenya wote kudumisha amani na kuisaidia serikali kufanikisha miradi yote ya maendeleo saw ana ahadi ambazo imetoa kwa wakenya ili kuinua kiwango cha ukuaji wa uchumi itakayoivusha Kenya kutoka taifa linalostawi hadi lililostawi.’’
Akihutubia mkutano huo wa maaskofu, waziri wa Jinsia, Utamaduni, Sanaa na Urithi Hannah Wendot kwa upande wake aliyataka makanisa nchini kuwafahamisha washiriki wake kuhusu miradi ya serikali.
‘’Tunategemea kanisa Pamoja na wahikadau wengine kuweza kuzungumza na umma kupitia majukwaa yao huku pia sisi tukifanya hivyo kama serikali kueleza kuhusu miradi mingi ambayo serikali inaendeleza mfano mradi wa ujenzi wa makazi nafuu inayoendelezwa katika kila kaunti.’’ Waziri Wendot alirai.






