Mahakama kuu imedinda kumpa dhamana aliyekuwa mkuu wa kituo cha polisi cha Central Jijini Nairobi Samson Talaam kuhusiana na mauaji ya mwalimu na mwanablogu Albert Ojwang’.
Talaam na watuhumiwa wengine watano wakiwemo maafisa wa polisi wanakabiliwa na kesi ya mauaji ya Ojwang’ akiwa kizuizini katika kituo hicho.
Akitoa uamuzi wake siku ya Jumanne 30 Septemba 2025, hakimu Diana Kavedza aliamuru kwamba Talaam, James Mukhwana na Peter Kimani ambao ni maafisa wa polisi wa cheo cha konstebo pamoja na watuhumiwa wengine watatu wasalie kizuizini hadi pale ambapo mashahidi wakuu wa upande wa mashtaka watakapo toa Ushahidi.
“Kanuni za utoaji dhamana au bondi zinatambua kwamba haki hiyo inaweza kuzuiliwa iwapo huenda ikahujumu imani ya umma katika upatikanaji wa haki.’’ Jaji Kavedza aliamua.
Zaidi alihoji kwamba kuwaachilia kwa dhamana maafisa hao huenda kukachochea maandamano mengine na kuhatarisha usalama wao wenyewe.
Sita hao wanatuhumiwa kuhusika katika kupanga njama ya kudhulumiwa na kuuawa kwa Ojwang’, aliyeripotiwa kuaga dunia tarehe 8 Juni 2025 siku mbili baada ya kukamatwa nyumbani kwao kaunti ya Homa Bay na kusafirishwa hadi jijini Nairobi alikozuiliwa katika kituo cha polisi cha Central.