Odhiambo ajiondoa kwenye jopo la kuangazia fidia kwa waathiriwa wa maandamano

0

Rais Wa chama cha wanasheria nchini (LSK) Faith Odhiambo amejiuzulu kwenye jopokazi lililobuniwa kutadhmini na kupendekeza fidia kwa waathiriwa wa maandamano nchini.

Kujiuzulu kwa Odhiambo kulifuatia mashinikizo kutoka kwa baadhi ya wakenya na makundi mbalimbali yaliyoibua maswali kuhusu jopokazi hilo wakidai kuwa lilitwikwa jukumu la tume ya kitaifa ya kutetea haki za kibinadamu (KNCHR).

Kulingana na Odhiambo hatua yake ya Jumatatu tarehe 6 Oktoba ilitokana na kesi iliyowasilishwa mahakamani kupinga uhalali wa jopokazi hilo sawa na nafasi aliyokuwa akishikilia katika chama cha LSK.

“Jinsi mambo yalivyo jukumu la jopo lililokuwa litekelezwe ndani ya muda uliotengewa limesitishw ana mahakama, na kuna uwezekano wa muda huo kutamatika kabla ya kesi kuamuliwa,” alihoji Odhiambo.

Jopo kazi hilo liliteuliwa na rais William Ruto tarehe 25 Agosti kupitia notisi kwenye gazeti rasmi la serikali na kupewa muda wa siku mia moja ishirini kuwasilisha mapendekezo ya fidia kwa waathiriwa wa ukatili wa maafisa wa usalama sawa na ghasia za maandamano yaliyoongozwa na vijana wa kizazi cha Gen Z mwaka wa 2024 na 2025 ambapo baadhi waliaga dunia na wengine kujeruhiwa.

Odhiambo alikuwa naibu mwenyekiti wa jopokazi hilo chini ya uongozi wa mshauri wa rais Ruto wa masuala ya kisiasa Prof. Makau Mutua.

Odhiambo amekuwa mwanachama wa pili kujiuzulu kwenye jopokazi hilo baada ya mwanaharakati Irungu Houghton.

 

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here