Gavana wa kaunti ya Nyamira Amos Nyaribo amebanduliwa uongozini kutokana na tuhuma za matumizi mabaya ya mamlaka.
Katika kikao cha Jumanne tarehe 25 Novemba 2025 wakilishi wadi 23 walipiga kura kumwondoa ofisini gavana Nyaribo baada ya kujadili hoja ya kumbandua.
Kupitia hoja iliyokuwa imewasilishwa na mwakilishi wa wadi ya Bonyamatuta Julius Matwere, Nyaribo alituhumiwa kwa matumizi mabaya ya ofisi, uteuzi kinyume na sheria sawa na matumizi mabaya ya fedha za umma.
Alitangaza kubanduliwa kwa Nyaribo spika wa bunge la kaunti hiyo Thaddeus Nyarabo baada ya matokeo ya kura hizo.
‘‘Bunge la kaunti hii limeidhinisha kubanduliwa ofisini kwa Amos Nyaribo gavana wa kaunti ya Nyamira kwa tuhuma za ukiukaji wa katiba ya Kenya na sheria nyingine pamoja na matumizi mabaya ya ofisi.’’
Hili ni jaribio la tatu la kubanduliwa kwa Nyaribo ambaye alichukua hatamu ya uongozi baada ya kifo cha mtangulizi wake John Nyagarama akiepuka shoka mara mbili mwaka wa 2023 na 2024.
Nyaribo atasubiri hatua itakayofuata ambapo atalazimika kujitetea mbele ya maseneta watakaojadili hoja hiyo na kuamua iwapo watadumisha uamuzi wa kaunti au kuitupilia mbali.
Kisheria, spika wa bunge la kaunti atahitajika kumjuza spika wa bunge la seneti ili aweze kuratibu kikao cha kusikiliza shutuma dhidi ya gavana aliyebanduliwa.









