Wabunge kutoka kaunti ya Nairobi wameeleza kutoridhishwa na mpangilio wa usajili wa mwaka 2025 wa makurutu kujiunga na vikosi vya jeshi ulioratibiwa kuanza mwezi Oktoba wakidai ni baguzi.
Wakiongozwa na seneta Edwin Sifuna walidai kwamba wenyeji wa kaunti ya Nairobi walikuwa wamebagulia katika shughuli hiyo kutokana na kuratibiwa kufanyika kwake katika maeneo matatu pekee.
Kulingana nao, tofauti na kaunti nyingine ambapo shughuli hiyo iliratibiwa kufanyika katika kila eneo bunge, jijini Nairobi maeneo bunge yalikuwa yameunganishwa usajili ukipangiwa kufanyika katika maeneo matatu.
Walilalamika kwamba licha ya kumwandikia barua waziri wa ulinzi Soipan Tuya kuhusu hilo hakuna hatua iliyokuwa imechukuliwa wakitishia kutatiza mchakato mzima hadi kilio chao kisikilizwe.
‘’Tunachomwambia waziri ni kwamba tunaenda kuwasilisha hoja dhidi yake. Tulimwandikia barua, hajatujibu na tunataka atuambie ni nini hii ubaguzi dhidi ya Nairobi,’’ Mark Mwenje mbunge wa Embakasi Magharibi alisema.
‘’Iwapo hili halitabadilika tutasitisha usajili wa makurutu wa maafisa wa KDF nchini kote hadi kaunti ya Nairobi ipewe nafasi sawa na kaunti nyingine 46’’
Katika usajili huo utakao anza mwezi Oktoba, Idara ya ulinzi ilitangaza kwamba jijini Nairobi utafanyika katika uwanja wa Nyayo, Kasarani na Jamhuri.