Mtawa Aliyekuwa Akizuiliwa Kuhusiana na Mauaji Sasa Kuwa Shahidi wa Serikali

0

Mtawa wa Kanisa Katoliki, Caroline Kanjiru, ambaye awali alizuiliwa na polisi kwa tuhuma za kuhusika katika mauaji ya mwenzake, sasa ameondolewa lawama na anatarajiwa kuwa shahidi wa upande wa mashtaka huku uchunguzi kuhusu kifo hicho ukiendelea.

Marehemu Mtawa Anselmina Karimi, mwenye umri wa miaka 65, ambaye alikuwa msimamizi wa Kituo cha Watoto cha Nkabune mjini Meru, alipatikana amefariki dunia nyumbani kwake mnamo Oktoba 12, 2025, akiwa na jeraha kichwani na damu ikitoka.

Baada ya tukio hilo, Mahakama ya Meru ilikubali ombi la Idara ya Upelelezi wa makossa ya Jinai (DCI) kumweka kizuizini Kanjiru kwa muda wa siku 14 katika Kituo cha Polisi cha Meru ili kuruhusu uchunguzi zaidi, ikiwemo uchambuzi wa data za simu na uchunguzi wa Msimbojeni (DNA).

Hata hivyo, wakati kesi hiyo iliporejelewa mahakamani Oktoba 28, 2025, afisa mpelelezi kutoka makao makuu ya DCI, Patrick Wachira, aliiarifu mahakama kuwa uchunguzi uliofanyika hadi sasa haujampata Mtawa Kanjiru na uhusiano wowote na mauaji hayo.

“Kutokana na uchumbuzi wa rekodi za data za simu pamoja na kuwahoji mashahidi imebainika kwamba mshukiwa hana uhusiano wowote na mauaji hayo,” Wachira aliiambia Mahakama.

Kwa mujibu wa Wachira, uchunguzi bado unaendelea ili kubaini watu waliohusika moja kwa moja na mauaji ya Mtawa Karimi.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here