Mahakama ya ajira imefutilia mbali mchakato wa usajili wa makurutu 10,000 wa polisi.
Kwa mujibu wa Jaji Hellen Wasilwa Tume ya huduma za polisi haina uwezo wa kuwapandisha vyeo au kuwafuta kazi maafisa wa polisi.
“Jukumu la kuajiri, kutoa mafunzo, kupanga majukumu, kuwasimamisha kazi na kuwafuta kazi maafisa wa polisi ni la huduma ya polisi ya kitaifa pekee,” amesema Jaji Wasilwa katika uamuzi wake.
Mahakama imebaini kuwa tume ya huduma ya polisi si chombo cha usalama wa taifa chini ya ibara ya 239 ya katiba na hivyo haina mamlaka ya kuendesha mchakato wa uajiri wa polisi.
Uamuzi huo umefutilia mbali tangazo la ajira lililotolewa na mwenyekiti wa tume hiyo Peter Lelei na kutangaza kuwa halina msingi wa kisheria pia imezuia kwa amri ya kudumu tume ya huduma ya polisi kuendelea na mchakato wowote wa uajiri, mafunzo au nidhamu ya maafisa wa polisi.









