Meneja wa kampuni moja ya kutoa mikopo kwa njia ya simu anakadiria hasara baada ya kutapeliwa shillingi million tisa na mshukiwa wa uchawi aliyejifanya mchungaji.
Victor Anane raia wa Ghana anadaiwa kumtapeli meneja huyo wa kike baada yao kukutana kwenye mtandao wa kuchumbiana.
Binti huyo amewaambia maafisa kutoka idara ya upelelezi nchini DCI kuwa mshukiwa aliyejitambulisha kuwa mchungaji alimhaidi kumsaidia apandishwe cheo kazini na pia kupata mali nyingi iwapo tu angempenda.
Bila ufahamu, mwanadada huyo ‘aliingia boksi’ ya mshukiwa ambaye alikamatwa jana nyumbani kwake mtaani Transview, Athi River na bidhaa zinazoaminika kuwa za uchawi kunaswa ndani ya nyumba yake.
Mwanadada huyo alifahamu katapeliwa alipomtumia mshukiwa pesa hizo na kupokea mwaliko wa kuenda nyumbani kwake na ndipo aliigwa na butwaa alipopata bidhaa hizo za uchawi.
Uhusiano wa kimapenzi baina yao uliishia kwenye idara ya DCI wakati mwanadada huyo alikimbilia usaidizi wa maafisa hao ili kupata hela zake alizompa mpenzi huyo tapeli.
Mshukiwa anatazamiwa kufikishwa mahakamani hapo kesho kufunguliwa mashtaka.









