Mahakama imemtoza faini ya shilingi laki moja dereva wa mbunge wa Kibra Peter Orero, George Oduor kwa kosa la kukiuka sheria za trafiki.
Hii ni baada ya Oduor kukiri mashtaka yakiwamo kuendesha gari kwa mkondo usiofaa sawa na kwa njia iliyowazuia na kuhatarisha maisha ya watumizi wengine wa barabara.
Dereva huyo aliyefikishwa katika mahakama ya Milimani Jumatatu 13 Oktoba alijipata pabaya baada ya video iliyomnasa akivunja sheria za trafiki siku ya Alhamisi tarehe 9 Oktoba kusambaa mitandaoni.
Mbele ya hakimu Rose Ndombi, Oduor alikiri mashtaka na kuomba msamaha akidai alikuwa mbioni kuelekea kwenye uwanja wa ndege wakati wa tukio.
‘‘Nilikua nakimbia katika uwanja wa ndege na kulikua na msongamano wa magari, nikaamua kuyapita magari mengine ili kuokoa muda. Ni mara yangu ya kwanza kuvunja sheria na sitarudia kosa hilo,’’ aliiambia mahakama.
Oduor alihitajika kulipa faini papo hapo au kutumikia kifungo cha mwaka mmoja gerezani kwa hatia ya kosa hilo.