Waziri Mkuu wa Haiti Ariel Henry amejiuzulu kufuatia ongezeko la shinikizo na ghasia nchini humo.
Tangazo la kujiuzulu kwake limetolewa na rais wa taifa la Guyana Irfaan Ali ambaye vilevile ndiye kiongozi wa muungano wa mataifa ya Karebia.
Magenge yenye silaha yameripotiwa kumzuia Henry kurejea nchini humo tangu alipozuru taifa la Kenya ili kutia saini mkataba wa kuruhusu Kenya kuwatuma maafisa wake wa polisi nchini humo.
Hatua hiyo ya kujiuzulu inajiri siku moja baada ya waziri wa masuala ya ndani nchini Kenya Prof. Kithure Kindiki kusisitiza kwamba serikali ya Kenya haitalegeza kamba katika kuwatuma maafisa wake wa polisi nchini Haiti ili kusaidia kuimarisha usalama.
Kindiki alisema mikakati ya kuwatuma maafisa hao imekamilika na hivi karibuni watajiunga na vikosi vingine vya usalama kuyakabili magenge ambayo yameripotiwa kulemaza shughuli mbalimbali katika taifa hilo la Carribean.
Kauli ya waziri Kindiki inajiri huku Marekani ikiendelea kuwaondoa maafisa wake wanaohudumu nchini Haiti kufuatia kudorora kwa usalama katika mji mkuu wa Port-au-Prince.
Magenge yenye silaha kali yamekuwa yakidhibiti mitaa ya mji mkuu wa Haiti Port-au-Prince katika siku za hivi karibuni, yakimtaka waziri mkuu huyo ambaye hakuchaguliwa kujiuzulu.
Henry amekuwa ungozoni tangu kuuwawa kwa rais wa zamani wa nchi hiyo Jovenel Moïse Julai mwaka wa 2021.