Watu wanne wa familia moja wafariki kwenye ajali ya barabarani Siaya

0
Gari lililoharibika kufuatia ajali barabarani
Gari lililoharibika kufuatia ajali barabarani

Watu wanne wa familia moja wamefariki katika ajali ya barabarani iliyohusisha gari aina ya saloon na basi la shule katika eneo la Kagoya, barabara ya Siaya-Nyadorera usiku wa kuamkia Jumatatu.

Wanne hao akiwemo baba na wanawe wawili (umri wa miaka 5 na 10) pamoja na msaidizi wao wa nyumbani walifariki papo hapo.

Kulingana na chifu wa lokesheni ya Usonga Paul Kanoti, familia hiyo ilikua ikitoka Siaya kuelekea Nyadorera walipokutana na mauti yao.

Gari hilo la kibinafsi lilikuwa likijaribu kupita lori lilipogongana na basi la shule ya Yogo Academy.

Kanoti ameambia vyombo vya habari kwamba wanne hao walifariki papo hapo huku mkewe jamaa aliyeaga na mtoto mwingine wakipata majeraha mabaya na kwa sasa wanapokea matibabu wakiwa hali mahututi.

Dereva wa basi hilo anapokea matibabu katika hospitali ya Rufaa ya kaunti ya Siaya.

Haya yanajiri wakati ambapo serikali imetangaza mpango wa kurejesha vifaa vya kupima viwango vya matumizi ya pombe miongoni mwa madereva, almaarufu Alco-blow.

“Tutaagiza vifaa vya Alco-blow 1000 kutusadia kugundua madereva walevi, hatua hii imetokana na maafa ambayo yameendelea kuongezeka.” Waziri wa Uchukuzi Davis Chirchir alitangaza siku ya Jumapili.

Wiki jana pekee makumi ya watu walipoteza maisha katika ajali ya barabarani katika sehemu mbalimbali za taifa; Kumi na tano wakiaga kwenye barabara ya Sotik- Kericho, na watano wakiwemo wanafunzi watatu katika eneo la Nyakach.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here