Huenda utapigwa faini iwapo utapatikana bila barakao katika mojawapo wa juhudi zinazowekwa na serikali kuzuia msambao wa virusi vya corona.
Haya yamesemwa na waziri wa afya Mutahi Kagwe ambaye amesema kuongezeka kwa msambao wa virusi hivyo katika siku za hivi maajuzi kumesababishwa na watu kukosa nidhamu ya kufuata masharti yaliyotolewa kudhibiti msambao wa virusi hivyo.
Maambuki ya virusi hivyo nchini yamepindukia 52,000 baada ya watu 761 kuambukizwa katika muda wa saa Ishirini na nne zilizopita.
Hii inafikisha idadi ya maambukizi nchini kuwa 52,612 baada ya kupima sampuli 4,830. Watu 346 wamepona ugonjwa huo na kufikisha idadi hiyo kuwa 35,604.
Maafa yanayotokana na ugonjwa huo yanaendelea kupanda huku waziri wa afya Mutahi Kagwe akidhibitisha vifo vya watu 14 zaidi na kufikisha idadi ya maafa nchini kuwa 964.
Wagonjwa 35 wako kwa vyumba vya wagonjwa mahututi huku wengine 1,084 wakilazwa katika hospitali mbalimbali.
Maeneo ambayo yametajwa kama chanzo kikuu cha maambukizi hayo ni kuliko na mikusanyiko ya watu na maeneo ya burudani na mikahawa.
Kuongezeka kwa virusi hivyo nchini kumemsababisha rais Uhuru Kenyatta kuitisha kikao na magavana Jumatano wiki ijayo kujadili hatua zitakazochukuliwa kudhibiti maambukizi hayo.