Hukumu dhidi ya washukiwa wawili waliopatikana na hatia ya kupanga na kutekeleza shambulizi la kigaidi katika jumba la kibiashara la Westgate imeahairishwa hadi Ijumaa wiki ijayo.
Hakimu wa mahakama kuu ya Milimani Francis Andayi amehairisha kutoa hukumu hiyo kwani ripoti inayofaa kuongoza hukumu dhidi ya washukiwa hao Mohammed Abdi Ahmed na Hussein Hassan Mustafa haijakuwa tayari.
Afisa amayehusika katika kuandaa ripoti hiyo Peter Macharia ameiambia mahakama kuwa hawajamaliza kuchukua taarifa kutoka kwa wahanga wa shambulizi hilo la mwaka 2013.
Macharia ameagizwa kuwasilisha ripoti hiyo mahakamani mapema wiki ijayo kabla ya hakimu Andayi kutoa hukumu.
Mawakili wa washukiwa wamelalamikia kutekwa nyara kwa mshukiwa wa tatu Liban Omar aliyeachiliwa huru na upande wa mashtaka umeasema unachunguza kisa hicho.
Liban ambaye ni nduguye mmoja wa washukiwa waliopatikana na hatia alipotea saa chache baada ya kuachiliwa na mawakili wake wanasema alitekwa nyara na watu wasiojulikana.
Omar aliondolewa mashtaka na mahakama baada ya upande wa mashtaka kukosa kutoa ushahidi wa kutosha kudhibitisha kuwa alikuwa miongoni mwa waliopanga na kutekeleza shambulizi hilo.
Kundi la kigaidi la Al Shabaab ambalo lina uhusiano na maharamia wa Al Qaeda lilidai kuhusika kwenye shambulizi hilo la tarehe 21 Septemba mwaka 2013.