Mahakama ya Nakuru imeagiza kuwa washukiwa 14 waliokamatwa kuhusiana na mapigano katika eneo la Njoro wazuiliwe kwa siku 10 zaidi kuwezesha kukamilika kwa uchunguzi.
Hakimu mkuu Elizabeth Usui ameagiza kuwa washukiwa hao akiwemo aliyekuwa MCA wa wadi ya Nessuit Joseph Miangari kuzuiliwa katika vituo vya Polisi vya Bondeni na Njoro.
Washukiwa hao wataendelea kuzuiliwa baada ya mahakama hiyo kuridhia ombi la upande wa mashtaka uliotaka wasalie rumande ili kutoa muda wa kukamilika kwa uchunguzi.
Mapigano katika eneo hilo yamesababisha maafa ya watu watano na kuwajeruhi wengine 83 kwa mujibu wa mshirikishi wa usalama katika eneo la Bonde la Ufa George Natembeya.