Jamii ya Wanubi nchini Kenya inamtaka rais Uhuru Kenyatta kuitambua rasmi ili kuiwezesha kupata stakabadhi muhimu za kitaifa ikiwemo vitambulisho vya kitaifa.
Shirika la Nubian Rights Forum kupitia kwa mwenyekiti wake Shaffie Ali linasema kwa mfano imekuwa vigumu kwa vijana wa jamii hiyo kujiunga na mpango unaoendelea wa kazi mtaani kwa sababu hawana vitambulisho vya kitaifa.
Aidha wamelalamikia ukaguzi wanaofanyiwa ili kupata vitambulisho jambo wanalolitaja kama ubaguzi.
Jamii hiyo iliingia Kenya zaidi ya miaka hamsini iliyopita na waliletwa kutoka Sudan na iliyokuwa serikali ya mkoloni kuwafanyia kazi.
Hadi wakati huu, watu zaidi ya laki moja kutoka jamii wameendelea kuiomba serikali kuwatamabua kama Wakenya bila kufua dafu.