Wanasiasa wanaendelea kulaumiwa huku maafa yaliyotokea Jumapili katika eneo la Kenol, Murang’a yakibakia kuwa kitendawili.
Kinara wa chama cha ODM Raila Odinga amewasihi viongozi kukomesha kampeini za mapema huku akisema ghasia kama zile zilizoshuhudiwa Murang’a kwa muda mrefu zimelitumbukiza taifa la Kenya katika uhasama wa mara kwa mara.
Waziri huyo mkuu wa zamani ameonya kuwa mbegu ya vurugu inayopandwa wakati huu miaka miwili kabla ya uchaguzi mkuu ina uwezo wa kichupuka tena na kusababisha madhara makubwa kwa taifa.
Mbunge wa Kiharu Ndindi Nyoro amekana kuhusika kwa vyovyote na vurugu zilizotokea katika eneo la Kenol, Murang’a ambapo watu wawili waliuawa na wengine kupata majeraha.
Badala yake mbunge huyo mwendani wa naibu rais William Ruto ameilaumu serikali kwa kupanga rabsha hizo ili kuvuruga mikutano ya Ruto.
Wakati uo huo baadhi ya wabunge wakiongozwa na Junet Mohamed wa Suna Mashariki na John Mbadi wa Suba Kusini wamemlaumu naibu rais William Ruto kutokana na kile wametaja kama kuwatumia wendani wake kuzua vurugu.
Nyoro pamoja na mwenzake wa Kandara Alice Wahome wametakiwa kufika katika afisi za idara ya upelelezi DCI kurekodi taarifa kuhusiana na vurugu hizo.
Wakati uo huo
Mamlaka ya Usalama barabarani NTSA imeagiza maafisa wa kampuni mbili za uchukuzi wa umma za Neo Kenya Mpya na Joy Kenya kufika mbele yao kuhusiana na vurugu za Kenol kaunti ya Murang’a.
Katika taarifa, NTSA inasema maafisa hao watatoa mwanga zaidi kuhusiana na vurugu hizo na iwpao mabasi yao yalihusika.
Inadaiwa kuwa mabasi ya kampuni hizo mbili yalitumika kusafirisha wahuni waliozua vurugu kabla ya hafla ya kuchangisha pesa iliyoongozwa na naibu Rais William Ruto.