Watu wanaoougua magonjwa yasiyo ya kuambukiza nchini Kenya (NCDs) wamelalamikia kubaguliwa na serikali wakati huu taifa linapokabiliana na janga la COVID19.
Watu hao wanaugua magonjwa kama vile kisukari, saratani, magonjwa ya kupumua na magonjwa ya kupumua wanasema imekuwa vigumu kwa wao kuhudumiwa katika hospitali za umma kwa sababu waliopata ugonjwa wa corona ndio wanapewa kipau mbele ilhali wao wanapuuzwa.
Hili wanasema linahatarisha maisha yao kwani wanasema wako hatarini kupatwa na matatizo makubwa zaidi kiafya ambayo huenda yakasababisha maafa.
Ni kutokana na changamoto hizi ndiposa watu hao wanaiomba serikali kuyapa kipaumbele mahitaji na huduma kwa watu walio na magonjwa yasiyoambukiza kwa kuhakikisha kwamba wanawekwa kwenye mstari wa mbele katika kupambana na janga la COVID-19 nchini Kenya.
Leah Kilenga ni mmoja wa wanachama wa taasisi inayoshughulikia watu wanaougua magonjwa yasioambukizwa (PLWNCDS) nchini.
Kuu zaidi ni kwamba serikali iboreshe mfumo wa ugavi wa dawa na bidhaa muhimu za magonjwa yasiyoambukiza; kuhakikisha kwamba dawa na bidhaa hizi zinapatikana kwa urahisi wakati wote na kwa bei nafuu katika vituo vya msingi vya afya; na vilevile kuhakikisha kwamba watu wanaoishi na magonjwa yasiyoambukiza ambao hawawezi kufika kwenye maduka ya dawa au hospitali wanapokea huduma hizi.