Waliokula pesa za corona washikwe asema Karua

0

Chama cha NARC Kenya kinamtaka Rais Uhuru Kenyatta kuwatia mbaroni na kuwashtaki maafisa wakuu serikalini ambao wanadaiwa kula pesa zilizonuiwa kupambana na janga la corona.

Kiongozi wa chama hicho Martha Karua anasema hakuna uwazi kwenye matumizi ya pesa hizo na anamtaka rais kujitokeza bayana kuwachukulia hatua wahusika.

Wakati uo huo Karua anamtaka Rais kuelekeza fedha zaidi katika sekta ya afya ili kupambana na janga la corona na pia kuhakikisha kuwa maslahi ya wahudumu wa afya yanatiliwa manani.

Haya yanajiri siku moja tu baada ya waziri wa Afya Mutahi Kagwe kusema hatajiuzulu kutoa nafasi ya uchunguzi wa utumizi mbaya wa fedha za kupambana na janga hilo.

Nalo shirika la Transparency International (TI) pia limeelezea wasiwasi wake kuhusu matumizi ya pesa zilizotengwa kwa minajili ya kukabiliana na janga la corona.

TI kupitia taarifa inasema maswali yaliyoulizwa na bunge kuhusu zilivyotumika Sh1.3b bado hayajapata majibu huku Wakenya wakisalia gizani kuhusu ni vipi pesa hizo za mlipa ushuru zimetumika.

Katika mapendekezo yake, shirika hilo linaitaka serikali kuweka wazi maelezo kuhusu zilivyotumika pesa hizo kwa kuzingatia uwajibikaji.

TI vile vile imetoa changamoto kwa kila kaunti kuweka wazi pesa zilizotengwa hususan kukabiliana na janga hilo na iwapo lengo hilo limeafikiwa.

 

 

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here