Wakenya wakosa huduma za matibabu kwa siku ya pili mfululizo

0

Huduma za matibabu katika hospitali mbalimbali za umma kote nchini zimesambaratika kwa siku ya pili mfululizo kudfuatia mgomo wa wauguzi na maafisa wa kliniki.

Wagonjwa katika maeneo mbalimbali nchini waliofika hospitalini wamepatwa na mshangao wa kutohudumiwa na yeyote na kulazimika kutafuta huduma hizo muhimu katika hospitali za kibinafsi.

Katibu mkuu wa muungano wa wauguzi tawi la Kisumu Ann Owiti anawataka wakenya wasipeleke wapendwa wao wagonjwa katika hospitali za serikali kaunti hiyo kwani hawatapata huduma.

Katika kaunti ya Bungoma Wauguzi, matabibu na wahudumu wa maabara wameapa kuwa hawatarejea kazini iwapo lalama zao hazitashughulikiwa.

Katika kaunti ya Bomet, wauguzi wameandamana kushinikiza kupewa kile wanasema ni haki yao ikiwemo kulipwa mishahara kwa wakati, kupandishwa vyeo na kupewa vifaa vya kujikinga dhidi ya maambukizi ya corona.

Mjini Mombasa, Katibu mkuu wa muungano wa wauguzi KNUN katika kaunti hiyo Peter Maroko anasema wauguzi ambao wamekuwa kwenye mgomo kulalamikia kupuuzwa na serikali ya Gavana Ali Hassan Joho wanaendelea pia na mgomo wa kitaifa kushinikiza kupewa mishahara ya hadi miezi sita, kando na matakwa mengine.

Katika kaunti ya Busia, wahudumu hao wanasema baadhi yao hawajapokea mshahara kwa muda wa miezi tisa.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here