Wakenya 316 wafariki dunia wakifanya kazi katika mataifa ya mashariki ya kati.

0
Waziri mwenye mamlaka makuu pia masuala ya kigeni Musalia Mudavadi akiwa mbele ya bunge la seneti.

Wakenya 316 wamefariki dunia wakifanya kazi katika mataifa ya mashariki ya kati tangu mwaka wa 2002.

Ndizo takwimu za wizara ya masuala ya kigeni kama zilivyowasilishwa bungeni na waziri Musalia Mudavadi akiweka wazi kuwa jumla ya wakenya 416,548 wanafanya kazi katika mataifa sita miongoni mwa manane ya mashariki ya kati.

Aidha katika kikao hicho cha seneti, Maseneta wakiongozwa na Issa Juma wa kaunti ya Lamu walizilaumu balozi za Kenya katika mataifa hayo kwa kutowajibika kuhusu maslahi ya wakenya wanaoishi nje ya nchi wakilalamikia ugumu wakati wa kufuatilia chanzo cha vifo vyao vinapotokea.

Akijibu maswali ya maseneta, Mudavadi anayeongoza wizara ya mambo ya kigeni amesema kuwa panapotokea kifo, wizara hiyo husimamia maswala tofauti tofauti yakiwemo kutafuta stakabadhi na mali ya aliyeaga dunia na kutoa ushauri katika hatua zote za kuhakikisha kwamba mwili wa aliyeaga umesafirishwa kuja nchini.

Hata hivyo Mudavadi ambaye pia ni waziri mwenye mamlaka makuu alieleza kwamba serikali huwa haina uwezo kikamilifu wa kushughulikia gharama zote zinazojitokeza.

Hata hivyo alieleza ni vigumu kutoa utambulisho wa watu hao kwa sababu baadhi yao hawajajisajili na ubalozi wa Kenya katika mataifa hayo.

Aliongeza kuwa wengine pia huhama kutoka nchi hadi nchi, jambo ambalo pia ni vigumu kulifuatilia bila kusajiliwa.

 Kwa mujibu wa deta zilizotolewa na wizara ya masuala ya kigeni kuhusu vifo vya wakenya ni kwamba vifo 166 vimenakiliwa nchini Saudi Arabia, Qatar 58, Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE) 51, Iraq 25, Bahrain 10, Kuwait 6.

Mudavadi pia alisema kwamba serikali imekuwa ikifuatilia kwa karibu hali ya wananchi wake walioko nje ya nchi na kutoa msaada kwa familia zilizofiwa.

Wizara hiyo ilibainisha kuwa taifa la Saudi Arabia ndilo linaloongoza kwa idadi kubwa ya wakenya wanaofanya kazi huko ambao ni watu 310,266.

Qatar ni ya pili kwa kuwa na wakenya 66,025, UAE ya tatu ikiwa na Wakenya 23,000, Bahrain ina wakenya 8,000, Oman 5,392, Kuwait 3,515, Iran 200, na Iraq 150.

 

 

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here