Zaidi ya wakenya 149,000 wamefanikiwa kupata ajira katika mataifa ya Ughaibuni chini ya miaka miwili iliyopita.
Haya yamebainishwa na msemaji wa serikali Dkt Issac Mwaura ambaye amesema kwamba 12,000 kati yao wamepata ajira kati ya mwezi November na Disemba mwaka huu.
Kwenye kikao chake cha kila wiki na wanahabari, Dkt. Mwaura amesifia mpango wa utawala wa sasa wa kazi Mtandaoni ambao kulingana naye umezalisha nafasi za ajira 243,000.
Akianisha mafanikio ya utawala wa Kenya kwanza katika mwaka wa 2024, Dkt. Mwaura amesema utawala wa Rais Willam Ruto umefanikiwa kusisimua uchumi kwa kutoa mikopo kupitia hazina ya Hustler fund.
” utawala wa Rais Ruto umesambaza zaidi ya shilingi Bilioni 60 kupitia Hustler fund. Tumefanikiwa kuwaondoa wakenya kwa minyororo ya mikopo ya riba ya juu”. Mwaura amedokeza.
Serikali aidha imetetea utendakazi wake katika sekta ya afya ikisema imerahisisha upatakinaji wa afya mashinani kupitia Wahudumu wa afya wa Jamii almaarufu CHVs.
Aidha imesema idadi kubwa ya wakenya wamefanikiwa kupata huduma za afya kupitia mpango wa SHA uliozinduliwa miezi miwili iliyopita.
“Zaidi ya wakenya milioni 16.5 wamejisajili kwa SHA idadi hii ikijumisha waliohamishwa kutoka NHIF”, amesema Mwaura.