Wafanyikazi wa vyuo vikuu vya umma humu nchini pamoja na wahadhiri wametangaza kuanza rasmi kwa mgomo wa kitaifa wakishikilia kutolegeza msimamo hadi matakwa yao yatakapotekelezwa.
Kupitia Muungano wa Wahadhari Humu Nchini (UASU) na Muungano wa Wafanyikazi wa Vyuo Vikuu (KUSU) wafanyikazi hao wakiongozwa na Mwenyekiti wa UASU Jacob Musembi wameinyoshea serikali kidole cha lawama kwa kucheleweshwa kwa mazungumzo ya kujadili makubaliano ya pamoja ya 2021 – 2025.
“Tuliongeza muda wa makataa ili kutoa nafasi kwa serikali na waajiri wetu ili kutafuta suluhu ila hakuna kilichofanyika ndio sababu tumeamua kugoma, tuko hapa kuanzisha rasmi mgomo wetu tukiwaamuru wanachama wetu kote nchini kushiriki katika mgomo huu kuanzia asubuhi ya leo hadi makubaliano yatakapoafikiwa,” aliamrisha Musembi.
Wakizungumza na wanahabari wakati wa kutangaza mgomo huo katika Chuo Kikuu cha Kiufundi cha TUK jijini Nairobi, wafanyakazi pamoja na wahadhiri wamelalamikia malipo duni, kucheleweshwa kwa mishahara, kutowasilishwa kwa makato pamoja na changamoto za bima ya matibabu.
Hata hivyo japo wameeleza utayarifu wao wa kushiriki mazungumzo ya kutafuta mwafaka wameapa kutorejea kazini kabla ya makubaliano kuafikiwa.
Hatua hii ya mgomo itakayosababisha shughuli za kawaida katika vyuo vikuu nchini kutatizika imejiri baada ya makataa yaliyokuwa yametolewa kwa serikali kutatua masuala yaliyoibuliwa kukamilika bila suluhu.