Maelfu ya watu wenye matatizo ya akili wamefungwa kwa minyororo katika maeneo mengi duniani, Shirika la Human Rights Watch limesema kwenye ripoti iliyotolewa Jumanne.
Wanaume, wanawake na watoto wenye tatizo hilo baadhi wakiwa wa umri mdogo wa miaka 10 hufungwa kwa minyororo kwenye vyumba au mahala palipozingirwa, kwa wiki kadhaa, miezi au hata miaka.
Audry Wabwire mkurugenzi wa mawasiliano katika shirika hilo kanda ya Afrika Mashariki anasema hii ni hali inayoziathiri karibu nchi 60 barani Asia, Afrika ikiwemo Kenya, bara Ulaya, Mashariki ya kati na Amerika.
Ripoti hiyo yenye kurasa 56 inaangazia namna familia huwafungia nyumbani watu wenye maradhi ya akili au kuwazuia kwa lazima kwenye makao machafu tena yenye msongamano wa watu huku wakiwa wamefungwa minyororo.
Hii ni kutokana na unyanyapaa na sifa mbaya ambayo familia huipata katika jamii punde inapojulikana kwamba ina jamaa wa maradhi ya akili. Vilevile kuna ukosefu wa matibabu katika nchi nyingi.
Waathiriwa wengi hulazimika kula, kulala, kwenda haja ndogo na kubwa pale walipofungiwa. Katika vituo vya serikali, vituo binafsi au vituo vya kijamii na kidini vya kuwatibu watu wenye matatizo ya akili, watu hao hulazimika kufanya mfungo wa kwenda bila chakula, kunywa dawa nyingine ikiwa ya kienyeji, huku wakipigwa au kudhulumiwa kimapenzi.