Kama hamtulipi hatufanya kazi, ndizo kauli zinazotolewa na wafanyikazi wapatao 5, 000 katika hospitali ya rufaa ya Kenyatta (KNH) ambao wameandamana hii leo kulalamikia kutolipwa mishahara na marupurupu yao.
Wafanyikazi hao wametekeleza tishio lao la kuandamana hadi katika afisi za tume ya kuratibu mishahara ya watumishi wa umma (SRC) jijini Nairobi ambapo wameishutumu tume hiyo kwa kuhujumu utekelezwaji wa makubaliano yaliyoafikiwa mwaka 2012.
Lalama kuu za wafanyikazi hao ni kwamba hospitali hiyo ilipandishwa hadhi hatua iliyomaanisha kwamba wanapaswa kupewa nyongeza ya mishahara ila hilo halijafanyika miaka saba baadaye.
Nao matabibu katika kaunti ya Bomet wametishia kugoma iwapo serikali ya kaunti hiyo haitashughulikia malalamishi yao yanayojumuisha mazingira bora ya kufanyia kazi.
Katibu mkuu wa maafisa hao wa kiliniki katika hospitali ya Longisa Kipkoech Timothy amesema kuwa tangu mwaka wa 2013 zaidi ya matatibu 55 hawajapokea nyongeza ya mishahara wala kupandishwa vyeo.