Tume ya huduma za bunge PSC imeapa kuelekea mahakamani kupinga ushauri wa jaji mkuu David Maraga kwa Rais Uuru Kenyatta kulivunja bunge kwa kushindwa kupitisha mswada wa uwakilishi sawa wa jinsia.
Mwenyekiti wa tume hiyo spika Justin Muturi amesema ushauri huo wa Maraga kwa Rais unakiuka katiba na kudai kuwa amefanya uamuzi huo kwa pupa kwani kuna kesi mahakamani kuhusiana na kuvunjwa kwa bunge.
Muturi amesema kwa sasa taifa haliko tayari kuenda kwa uchaguzi na kumshtumu Maraga kwa madai ya kutaka kulitumbukiza taifa kwenye mgogoro wa kikatiba.
Ushauri wa mawakili
Hata hivyo Rais wa muungano wa mawakili nchini LSK Nelson Havi anamtaka Rais Uhuru Kenyatta kulivunja bunge kwa muda wa siku 21 zijazo kufuatua ushauri wa jaji mkuu David Maraga.
Havi anasema kuanzia hii leo wabunge hawafai kupokea mishahara na kuwa miswada yeyote ambayo watapitisha kuanzia leo haitokuwa na maana kwani watakuwa wanafanya vikao kinyume cha sheria.
Kwenye ushauri wake, Maraga alimtaka Rais Uhuru Muigai Kenyatta kulivunja bunge kuambatana na katiba kwa kushindwa kupitisha sheria ya uwakilishi sawa wa jinsia.