Zaidi ya wabunge 300 kutoka vyama vya Jubilee na ODM wamekubaliana kuunga mkono ripoti ya BBI baada ya mkutano ulioongozwa na rais Uhuru Kenyatta na mwenzake Raila Odinga.
Kwenye taarifa iliyosomwa na kiongozi wa walio wachache katika bunge la Senate aliye pia seneta wa Siaya James Orengo, wabunge hao wanaokutana mjini Naivasha wameafikia kuzuru maeneo mbalimbali kote nchini kuipigia debe ripoti hiyo.
Kwa mujibu wa ratiba ya kuelekea kwa kura ya maamuzi mwaka ujao, shughuli nzima ya kukusanya sahihi milioni moja itaanza Novemba 2 na kuendelea hadi Disemba 2 mwaka huu.
Mswada kuhusu kubadilishwa katiba utakuwa tayari kufikia Disemba 9 kabla ya tume ya uchaguzi IEBC kutathmini sahihi hizo kati ya Disemba 10 na Januari 10, mwaka ujao 2021.
Kati ya Januari 11 na 18, IEBC itawasilisha sahihi hizo kwa mabunge ya kaunti ambayo yatakuwa na hadi Februari 19 kuidhinisha mswada huo.
Kisha bunge litaidhinisha mswada huo katika ya Februari 20 na Aprili 5 kabla ya IEBC kuandaa kura maamuzi kati ya Aprili 6 na Juni 6.
Na huku Uhuru na Raila wakiongoza wabunge Naivasha kuunga mkono ripoti hiyo, naibu rais William Ruto anatoa wito wa kujumuishwa kwa maoni yote kinzani yanayotolewa kuhusu ripoti ya maridhiano BBI.
Kwa mujibu wa Ruto, upo uwezekano wa kukubaliana kuhusu maswala yenye utata kwenye ripoti hiyo na kuwezesha taifa kusonga mbele.