Wakenya wamelaumiwa kwa kulegeza masharti ya usalama na hivyo kusababisha kuanza kuongezeka kwa idadi ya visa vya ugonjwa wa corona.
Katibu katika wizara ya afya Dkt. Rashid Aman ametangaza kupatikana kwa visa vipya 442 baada ya kupima sampuli 5,327 na hivyo kufikisha idadi ya visa hivyo nchini kuwa 40,620.
Idadi ya maafa imeongezeka na kufikia 755 baada ya kufariki kwa watu 4 zaidi huku waliopona wakifikia 30,876 baada ya kupona kwa watu 166.
Dkt. Aman amewakumbusha Wakenya kuzingatia masharti ya usalama ikiwemo kuepuka mikutano ya kisiasa, kuvalia barakoa na zaidi kunawa mikono kila wakati.
Kaunti ya Nakuru kwa mara ya kwanza imeandikisha idadi kubwa ya virusi hivyo katika muda wa saa Ishirini na nne zilizopita baada ya kurekodi visa (94), Nairobi ni ya pili kwa visa (80), Mombasa (47), Uasin Gishu (22), Embu & Kisumu (20), Meru (15), Garissa (12), Kajiado (11), Kericho (10), Kwale (2) & Bungoma (1).
Na katika juhudi za kupambana na ugonjwa saratani, Dkt. Aman amezindua kituo cha kutibu ugonjwa huo katika kaunti ya Uasin Gishu huku akitaka kuwa saratani ya matiti inasababisha maafa watu 42,000 kila mwaka.