MAKUNDI mbalimbali ya kidini yanamtaka rais Uhuru Kenyatta kusitisha mara moja mikutano ya hadhara inayoendelea kupigia debe ripoti ya BBI.
Katika taarifa kwa vyombo vya habari, viongozi wa makundi hayo chini ya mwavuli wa Dialogue Reference Group wanahoji kuwa mikutano hiyo imesababisha uhasama nchini.
Wameongeza kuwa mikutano hiyo ya hadhara imeingilia majukumu ya jopokazi lililobuniwa kuangazia utekelezwaji wa ripoti hiyo na hivyo kufanya vigumu kwa wananchi kuelewa yaliyomo kwenye ripoti hiyo na kutoa mapendekezo yao.
Kwenye mapendekezo yao, makundi hayo yamemtaka rais Kenyatta kuanzisha mpango utakaohakikisha kuwa hamasisho limetolewa kwa Wakenya kikamilifu kuhusu ripoti hiyo na kufanikisha utekelezwaji wake.
Haya yanajiri siku chache baada ya viongozi wanaoegemea mrengo wa naibu Rais William Ruto kuondoka kwenye mkutano wa BBI kaunti ya Meru na kuwashtumu waandalizi kwa kile walisema ni “kuwatapeli wananchi.”
Viongozi hao pia wanataka wanasiasa kukoma kushambuliana kwa maneno hadharani na pia kukoseana heshima na kudai kuwa iwapo hilo litaendelea vizazi vijavyo vitaiga tabia ambazo hazifai.
Viongoiz hao pia wamemtaka Rais Kenyatta kujaza nafasi zilizoachwa wazi kwenye tume ya uchaguzi na mipaka nchini IEBC ili kuiwezesha kuratibu mipaka ifaavyo.