Ufisadi ndio kero kwa utendakazi wa idara za serikali – Koome

0

Jaji mkuu Martha Koome amekiri kuwa ufisadi umesalia kuwa changamoto inayohujumu utendakazi wa idara mbalimbali za serikali ikiwemo mahakama.

Jaji Koome alikiri kuwa visa kadhaa vya ufisadi ambavyo vimewahusisha majaji na maafisa wengine wa idara hiyo viliripotiwa katika baadhi ya mahakama nchini.

Akizungumza wakati wa kuzindua mkakati wa mwaka wa 2025 wa sekta ya haki katika kukabili ufisadi, Koome alisema kuwa idara anayoongoza itazidisha ushirikiano na tume ya maadili na kukabili ufisadi (EACC) pamoja na idara ya ujasusi ili kusaidia katika kuwatambua mapema maafisa wanaoendeleza ufisadi.

“Lengo letu ni kulinda uadilifu wa idara ya mahakama na kubuni hulka ambapo ufisadi huwezi kuendelezwa, ambapo ufisadi kwa kila hali utakuwa umepingwa,”

Katika hafla hiyo iliyofanyika jijini Nairobi, rais huyo wa mahakama ya upeo aliwataja wanaojihusisha na visa vya ufisadi kuwa wanaohujumu mchakato wa kuhakikisha kwamba kuna upatikanaji wa haki katika kesi mbalimbali ambazo zinawasilishwa mahakamani.

Kauli yake inajiri wakati ambapo idara ya mahakama nchini imeonekana kunyooshewa kidole na baadhi ya wakenya waliowasilisha malalamishi kwenye tume ya huduma za mahakama JSC wakitaka kuchunguzwa kwa baadhi ya majaji kwa madai ya utovu wa maadili.

Akisisitiza kujitolea kwa idara ya mahakama katika kukabili ufisadi Koome alidokeza kuhusu kuanzishwa kwa kamati za uadilifu katika mahakama zote ili kushughulikia changamoto za utoaji huduma katika ngazi za chini.

“Kamati hizi zitafanya kazi kwa bidii ili kubaini na kuziba mianya ya ufisadi inayoweza kutokea,’’ alisema Koome huku akiyarai mashirika mengine chini ya baraza la kitaifa la utawala wa haki (NCAJ) kubuni kamati zao binafsi za uadilifu.

 

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here